TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema fomu za
kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitaanza kutolewa
Agosti Mosi mwaka huu.
Kauli
hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian
Lubuva alipozungumza na waandishi wa habari
baada ya mkutano wa utiaji saini na vyama vya siasa katika Kitabu cha Maadili ya
Uchaguzi Mkuu.
Jaji
Lubuva alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali NEC itaanza lini kutoa fomu za
kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema
licha ya NEC kuanza kugawa fomu hizo za rais katika kipindi hicho, pia fomu za
wabunge zitatolewa Agosti 8 mwaka huu.
Akizungumzia
utiaji saini katika kitabu cha maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani,
alisema tume imekubaliana na vyama vyote 21 vilivyohudhuria mkutano huo wa
utiaji saini katika kitabu hicho isipokuwa Chama cha Wananchi (CUF).
“Tumekubaliana
baada ya kupitia maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa yakiihusu tume na kwa upande
mwingine vyama vya siasa, baadaye wote wakaridhia kuyatia saini,”alisema Jaji
Lubuva.
Alisema
CUF kimeshindwa kutokea katika utiaji saini huo kutokana na kukakabiliwa na
majukumu mengine na kusema kuwa chama hicho bado kina muda na wakati wowote
kinaweza kwenda kufanya hivyo.
Jaji
Lubuva alisema wahusika wakuu wa maadili hayo ni vyama vya siasa, wagombea,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na NEC, ambapo kila chama na
mgombea atawajibika kusaini maadili hayo.
“Chama
ambacho hakitasaini maadili haya kitazuiliwa kushiriki katika kampeni za
uchaguzi,”alisema Jaji Lubuva.
Alisema
kuwa kila mgombea atajaza na kusaini fomu na. 10 kuthibitisha kuwa ataheshimu
na kutekeleza maadili hayo na kwamba fomu hiyo itatolewa na NEC na kurudishwa pamoja
na fomu ya uteuzi.
Akizungumzia
kipengele cha mawasiliano ambacho kinasema hakuna mtu atakayeruhusiwa kutumia
simu ya kiganjani ndani ya kituo cha kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura
isipokuwa msimamizi wa kituo, wasaidizi wake na mlinzi wa kituo cha kupigia
kura.
“Watu
hao watatumia simu zao pale itakapobidi kwa shughuli za uchaguzi tu na simu
hizo wakati wote ziwe zimeondolewa mlio na ziwe kwenye mtetemo,”alisema Jaji
Lubuva.
Hata
hivyo, baada ya mvutano kuhusu kipengele hicho, NEC na vyama walikubaliana
mawakala waingie na simu, lakini wakati wote ziwe katika mtetemo huku mhusika
atakapohitaji kufanya mawasiliano atoke nje.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Salum Mwalimu
alisema kipengele hicho kimerekebishwa na kwamba kila wakala ataingia na simu
yake isipokuwa hawataruhusiwa kuongea ndani ya kituo cha kupigia kura.
Makubaliano
ya kusaini kitabu hicho cha maadili wiki iliyopita yalivunjika baada ya vyama
hivyo kubaini kuwa kurasa 10 kati ya 24 zilinyofolewa huku NEC ikishindwa
kuwafahamisha nini kilisababisha hali hiyo.
No comments:
Post a Comment