KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Friday 21 August 2015

TAMKO KUHUSU HALI YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
index
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HALI YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI

Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro. Ugonjwa wa kipindupindu katika mkoa wa Dar es Salam umeripotiwa katika Manispaa ya Kinondoni kuanzia tarehe 15 Agost, 2015. Tangu ugonjwa uanze hadi tarehe 20 Agosti 2015 idadi ya wagonjwa walioripotiwa ni 56 na vifo vya watu watatu (3). Wagonjwa walioathirika wanatokea maeneo ya Tandale, Mikocheni, Saranga, Kijitonyama, Makumbusho, Ubungo, Kigogo, Manzese, Kawe na Kimara katika Manispaa ya Kinondoni. Mkoani Morogoro wagonjwa nane (8) wameripotiwa na kifo cha mtu mmoja na wanatokea katika maeneo ya Kilakala na Mzinga Juu.
Kutokana na hali hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote wa nchini na hasa kwa mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na mikoa ya jirani.
Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kula chakula au kinywaji chenye vimelea vya “Vibrio cholera” ambavyo ndivyo husababisha ugonjwa wa kipindupindu. Vimelea hivi hupatikana kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kimechafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.
DALILI KUU ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU
Dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu ni pamoja na kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji meupe kama maji ya mchele na kunaweza kuambatana kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapataa huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji.

Hatua zilizochukuliwa
i. Kufungua kambi za wagonjwa wa kipindupindu katika Manispaa zote tatu za Dar es Salaam ambapo kwa Kinondoni kambi ipo Mburahati, Ilala kambi ipo kituo cha afya Buguruni na Temeke katika Hosipitali ya Temeke.
ii. Kutoa dawa, vifaa vya maabara na vifaa kinga 
iii. Kupima vipimo vya maabara na kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa
iv. Kupeleka timu za watalaam kutoka ngazi ya Mkoa na Taifa kusaidiana na timu za Manispaa husika. 
v. Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kuhusu ufuatiliaji na matibabu ya ugonjwa wa kipindupindu
vi. Kutoa elimu ya afya kwa jamii kuhusu namna ugonjwa unavyoenezwa na hatua za kuchukua ili kujikinga na maambukizo ya ugonjwa huu 
vii. Kutembelea maeneo yote walikotoka wagonjwa na kuhimiza kuzingatia kanuni za afya.
viii. Ufuatiliaji katika ngazi ya kaya walizotoka wagonjwa na pia kunyunyuzia dawa kwenye vyanzo vya maji (chlorine) na vyoo vya shimo na maji yaliyotuama
ix. Ukaguzi wa biashara za vyakula na vinywaji (Mama na Baba lishe).
x. Kushirikisha idara ya maji katika kuchukua sampuli kwenye vyanzo vya maji ya bomba na visima kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kimaabara. 
xi. Kuimarisha ukaguzi na upimaji wa afya za wauza vyakula katika migahawa na mama/baba lishe

Hata hivvo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa iliyoathiriwa itaendelea kufuatilia kwa karibu sana hali ya ugonjwa huu ili kuhakikisha kuwa ugonjwa huu unadhibitiwa mapema na kumalizika kabisa hapa nchini.
NJIA ZA KUDHIBITI KUENEA KWA UGONJWA HUU:
Wananchi wanashauriwa kuzingatia yafuatayo ili kujikinga na ugonjwa huu:
i. Epuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi 
ii. Nawa mikono yako kwa sabuni na maji safi kwa maji yanayotiririka:-
– kabla na baada ya kula
– baada ya kutoka chooni
– baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
– baada ya kumhudumia mgonjwa
iii. Epuka kusalimiana kwa kushikana mikono
iv. Kunywa maji yaliyo safi na salama – yaliyochemshwa au kutiwa dawa
v. Hakikisha mazingira yako yanakuwa safi wakati wote hasa chooni
vi. Usile tunda au kitu chochote bila kukisafisha kwa maji safi na salama
vii. Hakikisha unatumia choo kwa ufasaha na wakati wote
viii. Toa taarifa kituo cha Afya kilicho karibu na wewe endapo utapatwa na ugonjwa wa kuharisha au kutapika

Hitimisho
Wizara inapenda kuwatahadharisha wananchi kufuata kanuni za Afya, kama vile kunawa mikono na sabuni baada ya kutoka chooni na kabla ya kula chakula pamoja na kunywa maji yaliyo chemshwa au kutibiwa na dawa ya aina ya klorini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali 
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 20, August, 2015

No comments:

Post a Comment