KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Monday 18 January 2016

TTA YATAKA WAPANGAJI WAFIDIWE

CHAMA cha Wapangaji Tanzania (TTA), kinatarajia kutakutana na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba hivi karibuni, kuzungumzia hatima ya mali za wapangaji waliyokumbwa na bomoaboa katika nyumba zilizokuwa mabondeni.
Ripoti ya Serikali inaonesha kuwa hadi sasa nyumba  za wakazi  774 zimebomolewa, ambapo ni wakazi 20 tu ndiyo walikuwa na hati halali za makazi huku 119 wakiwa na leseni za makazi za muda mfupi.
Katibu Mwenezi wa TTA, Simon Kwezi, aliyasema hayo baada ya chama hicho kubaini kuwa serikali imeonesha kutoguswa na mahangaiko waliyoyapata wapangaji ambao ndiyo waliyokuwa wakiishi katika nyumba hizo na baadala yake imeamua kuwalipa fidia baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo.
Alisema, kabla ya kukutana na waziri huyo, chama hicho kimewataka wapangaji wote waliyokuwa wanaishi katika nyumba zilizokumbwa na bomoabomoa kujitokeza katika ofisi za chama hicho, kwa ajili ya kujiorodhesha kisha idadi yao akabidhiwe waziri huyo ili ikiwezekana serikali iwafidie.
Kwezi, alisema ili kupata orodha halali ya wapangaji hao, TTA imejipanga kufanya shughuli hiyo kwa kushirikiana na wenyeviti wa Serikali za Mitaa na wajumbe wakekatika maeneo yote ya jiji yaliyokumbwa na bomoabomoa hiyo.
“Tunaiomba serikali iwafidie wapangaji hawa kwani hawa ndiyo waliyoathirika zaidi katika bomoabomoa hiyo ukilinganisha na wa miliki kwani wao hawakuwa wakiishi katika nyumba hizo kutokana na kujua athari za kuishi maeneo hayo tangu awali.
“Tunajipanga kukutana na waziri ili kuona ni jinsi gani ya kuwasaidia wapangaji na endapo itashindikana kupatikama muafaka itawalazimu kwenda mahakamani kudai haki hiyo ambayo ni fidia,”alisema Kwezi.
Akizungumzia mikataba ya upangaji, alisema kuwa wapangaji wasikubali kuingia kwenye nyumba bila ya mkataba unaotambulika kisheria.
Alisema kitendo cha kuingia kwenye nyumba bila ya mkataba unaotambulika kisheria kimekuwa chanzo cha wamiliki hao kuongeza kodi mara kwa mara kwa wapangaji kutokana na tamaa binafsi ambazo zinasukumwa na uroho wa kipato.
“Tunawashauri kila wanapotaka kupanga wafike kwenye ofisi zetu popote katika maeneo husika ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria kwa chama chetu kinao wanasheria kwa ajili ya kupigania haki zenu,”alisema.
Kuhusu Madalali, Kwezi, alisema genge hilo limekuwa kikwazo kikubwa katika kupanda bei za upangaji wa myumba mijini.
“Hawa ni watu hatari kwani wamekuwa wakitumia ujanja wa kula kwa mpangaji na wamiliki, kwa hiyo ili kuepuka hayo ni vema wamiliki wakasajili nyumba zao katika ofisi za TTA ili kiweze kusimamia haki,”alisema.
Ili kukomesha magenge ya watu wachache wanaojiita madalali huku wakiwa hawana usajili wala hawalipi kodi serikalini, Kwesi alisema umefika wakati kwa serikali kuunda chombo kitakachopambana na magenge hayo ambayo huamua kuwalipisha wapangaji kodi ya kipindi cha miezi mitatu au mwaka jambo ambalo kisheria halikubaliki.

No comments:

Post a Comment