KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Saturday 20 February 2016

MAJALIWA AWATAKA WATANZAMIA KULIPA KODI HALALI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kampeni ya serikali ya awamu ya tano katika kupambana na baadhi ya watu  wanaopenda kufanya kazi kinyume cha sheria za nchi haina nia ya kumuoenea mtu.
Majaliwa, alisema mara baada ya kuanza kampemi hiyo inayoambatana na kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu, kumezuka manung’uniko kwa baadhi ya watu kutokana na hatua hizo zinazo chukuliwa na serikali katika kuwaajibisha watendaji wa umma na baadhi ya wafanyabiashara.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana, wakati wa Mkutano wa Wadau, wa kutoa taarifa ya hali ya kiuchumi na maendeleo ya Mkoa wa Rukwa na Katavi.
Majaliwa, alisema lengo la kampeni na kaulimbiu hiyo ya hapa kazi tu inalenga kuwakumbusha wananchi wote kuwajibika kwa bidii katika kila sekta husika ili kila mmoja azalishe vya kutosha ili kutunisha pato la taifa.
“Wote mnatambua kwamba ili kutimiza ahadi hizi ambazo viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano tumezitoa ni lazima tuwe na rasimali fedha za kutosha, napenda kusisitiza umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu na jukumu la kuchangia ili kupata fedha za kutosha kutuwezesha kutekeleza yale tuliyojipangia,”alisema Majaliwa.
Katika kusisitiza hilo, Majaliwa alisema kama ni mfanyabiashara lazima afanye biashara halali na kuhakikisha kuwa analipa kodi halali kwa serikali yake, kwamba serikali haitamvumilia mtu atakayejaribu kuzorotesha juhudi zinazofanywa na serikali katika upotevu wa mapato.
“Kama wewe ni mkulima lazima ulime kwa bidiii, uzalishe vya kutosha na mazao hayo yapate masoko, yauzwe na fedha zipatikane tulipe kodi ili kutuwezesha kutekeleza miradi hiyo.
“Kama ni mwana viwanda lazima kuzalisha bidhaa zenye ubora na bei yake iwe yakuridhisha kwa mtumiaji wa bidhaa hizo, lazima mwenye viwanda kulipa kodi halali kwa serikali kulingana na taratibu za kodi.
“Na kama wewe ni mtoa huduma za jamii iwe ni katika sekta ya Elimu, Afya, Maji na nyingine ni lazima kuhakikisha kwamba mnatoa huduma kwa kuzingatia maadili, kanuni na taratibu za kazi yako,”alisema Majaliwa.
Maliwa alitoa wito kwa Watanzania wote kwa kuwataka kumsaidia Rais John Magufuli ili aweze kutimiza la Kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu kwa weledi na maadili katika sehemu za kazi.
Akizungumzia kuhusu Kongamano hilo, Waziri Mkuu, alisema itaunga mkono kila azimio litakalopitishwa kwa ajili ya masilahi ya wananchi wa mikoa hiyo tena bila ya kuwaangusha kama ilivyowaahidi katika mikutano ya kampeni.
Aidha, alisema pamoja na fursa walizonazo bado kuna matatizo yanayohitaji kufanyiwa kazi kwani mikoa hiyo kwa muda mrefu haijawahi kuwa mikoa yenye ukame wa kutisha.
Alisema hiyo ndiyo sababu wafugaji wengi wametambua hilo na sasa wanaikimbilia mikoa hiyo.
“Tahadhali iliyoko ni kujiridhisha kama mifugo inayoingia kwa wingi kutoka mikoa na maeneo mengine inadhibitiwa, lazima kujiridhisha kwanza kama kasi ya mifugo inayoingia inaendana na maeneo yaliyotengwa rasni kwa ajili ya mifugo nay ale ya kilimo.
Tuchukue tahadhari mapema ya kutoanzisha migogoro ya wakulima na wafugaji katika mikoa hii,”alisema Majaliwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Ibrahim Msengi na mwenzake wa Rukwa kwa nyakati tofauti, walisema pamoja na mipango ya serikali bado Jumuiya ya Wanarukwa na Katavi wanaona vipaumbele, vikuu kwa maendeleo ya wananchi ambayo vinapaswa kusukumwa kwa kasi ya kutosha ni; Miundombinu ya barabara, maji, umeme, elimu, afya na uchumi.

MWISHO

No comments:

Post a Comment