KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 25 October 2017

Lugola: Tanesco, NEMC tunzeni bonde la Kihansi

NA MWANDISHI WETU, KILOMBERO

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, amelishauri Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutunza mazingira katika bonde la Kihansi.
Akiwa katika ziara ya siku moja kutembelea eneo hilo hivi karibuni, Lugola alisema ni wakati wa kuondoa dhana kuwa linapotajwa bonde la Mto Kihansi watu wanafikiria vyura adimu wanaopatikana katika bonde hilo tu duniani bali kuna masuala mengi yanayozunguka eneo hilo, ikiwemo vyanzo vya maji yanayotumika kuzalisha umeme.
“Mita moja ya ujazo ya maji inazalisha megawati saba za umeme, maana yake mkiyakosa haya maji hamtaweza kuzalisha umeme kama mnavyojisifia. Hivyo shirikianeni kwa pamoja kuhakikisha eneo hili la kilomita za mraba 580 mazingira yake hayaharibiwi, katika eneo hili kuna nyani, mbega na vipepeo wazuri lazima tuwalinde,” alisema Lugola.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NEMC, Dk. Vedast Makota, alisema kazi kubwa wanayoifanya ni kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo la Kihansi juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa sababu kila kilichokuwamo kina faida na kinategemeana katika ukuaji.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kihansi ya Chini (Lower Kihansi), Mhandisi Mathew Bundala aliishukuru NEMC kwa namna walivyokuwa karibu nao kuwaeleza baadhi ya masuala ya utunzaji wa mazingira na umuhimu wake, ameahidi kuyazingatia maagizo ya Naibu Waziri Lugola ili waendelee kunufaika na maji ya bwawa hilo.

No comments:

Post a Comment