KAMA UNA TUKIO LOLOTE LA KIJAMII, SIASA, UCHUMI TUWASILIANE KWA E-mail: shehesemtawa@gmail.com SIMU: 0719 352 268

Wednesday 25 October 2017

Meatu, Busega kukopa Bil. 17/-



NA COSTANTINE MATHIAS, SIMIYU

BARAZA ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Meatu mkoani hapa wameridhia kukopa Sh. Bil. 17.1 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
Maazimio hayo yalifikiwa katika kikao cha dharura cha baraza la madiwani vilivyofanyika kwa nyakati tofauti, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Busega imepanga kukopa Sh. Bil. 10.7 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa umwagiliaji.
Akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Mpango wa Kilimo cha Umwagiliaji wilayani Busega, Ofisa Mipango wa Wilaya hiyo, Josephat Joseph, alisema kuwa kazi za upimaji wa mashamba na njia ya kupita bomba la maji, kupima udongo, kusanifu mfereji mkuu kwenye chanzo, sehemu ya kuchukulia maji, nyumba za pampu, mifereji ya kuingiza na kutolea maji, kuandaa michoro na gharama za mradi zimeshakamilika.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo halmashauri ndiyo msimamizi mkuu na itajenga miundombinu na kuingia makubaliano na wakulima wa Mwamanyili kupitia umoja wao watakaounda. 
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, imepanga kukopa Sh. Bil. 6.4 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha Maziwa Meatu (Meatu Milk).
Akizungumzia upanuzi wa kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Fabian Manoza, wamekusudia kuongeza idadi ya wafugaji wanaopeleka maziwa kiwandani kutoka 45 wa sasa kufikia 400 wanaofuga ng’ombe wa kisasa.
Aliongeza kuwa mikakati mingine ni kununua mtambo mpya wa kuchakata maziwa lita 15,000 kwa siku, kununua mitamba 1,000 na kuandaa shamba la malisho lenye miundombinu muhimu pamoja na kuongeza soko. 

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema kuwa wamejipanga kutafuta majawabu ya changamoto za wafugaji kwa kuwasaidia kufuga kisasa, ikiwa ni pamoja na kuwashauri kupima maeneo yao na kuyawekea miundombinu muhimu kama mabwawa, visima, majosho na mashamba ya malisho.

No comments:

Post a Comment